Thursday, May 19, 2016

MAKUNDI KUWAPA YANGA ZAIDI MILIONI 300.

BAADA ya Yanga kufanikiwa kutinga hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho sasa klabu hiyo ina uhakika wa kuingiza kiasi cha dola 150,000 sawa na shilingi 327,900,000 au zaidi kulingana na hatua watakayoishia. Yanga ambayo imekuwa timu pekee kwa nchi za Afrika Mashariki kutinga hatua hiyo sasa inasubiri upangaji wa makundi ambao unatarajiwa kufanyika Jumanne Mei 24 mwaka huu. Katika hatua hii kutakuwa na timu nane ambapo mbali na Yanga lakini pia watakuwepo Etoile du Sahel ya Tunisia, TP Mazembe ya Congo DRC, Mo Bejaia ya Algeria, Madeama ya Ghana, Kawkab Marrakech ya Morocco, Al Ahly Tripoli ya Libya na Fus Rabat ya Morocco. Makundi yatakuwa mawili yenye timu nne nne ambapo mshindi wa kwanza na wa pili kutoka katika kila kundi ndio atakuwa amesonga mbele katika hatua nusu fainali. Bingwa wa michuano hii atajivunia kitita cha dola 625,000 sawa na shilingi 1,366,250,000 huku mshindi wa pili katika fainali akikunja kitita cha dola 432,000 sawa na shilingi 944,352,000. Mshindi wa pili na wa tatu kutoka katika makundi kila mmoja atapata dola 239,000 sawa na shilingi 522,454,000 na wa nne atakunja dola 150,000 sawa na shilingi 327,900,000.

No comments:

Post a Comment