MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Hispania, Fernando Torres amedai kuachwa kwake katika kikosi cha nchi hiyo kwa ajili ya michuano ya Euro 2016 hakujamzuia kujiandaa kwa kila kitu kwa ajili ya kuiongoza Atletico Madrid katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Torres ambaye hajaitumikia Hispania toka Kombe la Dunia mwaka 2014, amekuwa katika kiwango kizuri msimu huu huku mabao ake yakiisaidia klabu yake kumaliza katika nafasi ya tatu katika msimamo wa La Liga. Mbali na kuisaidia Atletico katika La Liga lakini pia ameisaidia kutinga hatua ya fainali ambapo sasa watakwaana na majirani zao Real Madrid Mei 28 mwaka huu katika Uwanja wa San Siro jijini Milan. Pamoja na kufunga mabao 12 msimu huu, Torres mwenye umri wa miaka 32 hakuchaguliwa katika kikosi cha awali cha kocha Vicente Del Bosque kwa ajili ya michuano ya Euro 2016 itakayofanyika huko Ufaransa mapema mwezi ujao. Akihojiwa Torres amesema hajali sana kuhusu Euro kwani ana mchezo mkubwa wa maisha yake atakaocheza hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment