Thursday, May 19, 2016

MKATABA MPYA WA NIKE WAIPA JEURI BARCELONA YA KUWAONGEZA MKATABA NEYMAR NA BUSQUETS.

KLABU ya Barcelona inadaiwa kuwa tayari imeanza kuweka sawa mipango yao ya baadae baada ya kutwaa taji lao la sita la La Liga katika kipindi cha miaka nane Jumamosi iliyopita. Utawala wa soka wa Barcelona nchini Hispania unaonekana hautaweza kuisha katika siku za karibuni kwani tayari wanadaiwa kufikia makubaliano ya mikataba mipya kwa nyota wake Neymar na Sergio Busquets pamoja na wadhamini wao kampuni ya vifaa vya michezo ya Marekani, Nike. Neymar anadaiwa kufikia makubaliano ya awali ya nyongeza ya mkataba ambao utadumu mpaka mwaka 2021 na kufanya nyongeza ya kuvunja mkataba huo kuongezeka mpaka kufikia dola milioni 213. Barcelona wana matumaini mkataba huo mpya Neymar atausaini kabla ya mchezo wao wa fainali ya Kombe la Mfalme dhidi ya mabingwa wa Europa League Sevilla. Kiungo Busquets pia anatarajiwa kusaini mkataba mpya ambao utamfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wanaolipwa zaidi katika orodha ya klabu hiyo. Yote hayo yanatarajiwa kuweza kufanikishwa kutokana na mkataba mpya watakaosaini na Nike ambao unakadiriwa kuwa na thamani ya dola milioni 112 kwa mwaka ukiwa unazidi ule wa Manchester United waliosaini na kampuni ya Adidas ya Ujerumani.

No comments:

Post a Comment