Tuesday, May 24, 2016

MAKUNDI KOMBE LA SHIRIKISHO: YANGA KUANZA UGENINI NA KUMALIZA UGENINI.

MABINGWA wa soka wa Tanzania, Yanga imepangwa kundi A katika ratiba ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho inayoandaliwa na Shirikisho la Soka la Afrika-CAF. Katika kundi hilo litakalokuwa na timu nne Yanga wamepangwa sambamba na Mo Bejaia ya Algeria, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-RDC na Medeama ya Ghana. Kundi B katika michuano hiyo litazikutanisha timu zote kutoka ukanda wa kaskazini mwa Afrika ambazo ni mabingwa watetezi Etoile du Sahel ya Tunisia, Ahly Tripoli ya Libya na Kawbab Athletic na FUS Rabat zote za Morocco. 
Kwa upande wa ratiba ya makundi michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kundi A limepangwa kuwa na timu za Zesco ya Zambia, Al Ahly ya Misri, Asec Mimosas ya Ivory Coast na Wydad Athletic ya Morocco. Kundi B litakuwa na timu za Enyimba ya Nigeria, Zamalek ya Misri, ES Setif ya Algeria na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ambao wamechukua nafasi ya AS Vita ya DR Congo ambao walitolewa kwa kucheza mchezaji asiyeruhusiwa. Timu hizo zitacheza na kila mmoja wapo nyumbani na ugenini huku washindi wawili kutoka katika kila kundi wakisonga mbele katika hatua ya nusu fainali. Mechi za makundi zinatarajiwa kuanza kuchezwa Juni 17 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment