Monday, March 28, 2016

HODGSON AMKINGIA KIFUA ROONEY BAADA YA VIJANA KUMFUNIKA.

KOCHA wa timu ya taifa ya Uingereza, Roy Hodgson amesisitiza nahodha wake Wayne Rooney bado yuko katika mipango yake kuelekea katika michuano ya Euro 2016 hata kama kikosi chake kiliwafunga mabingwa wa dunia Ujerumani bila uwepo wake. Mshambuliaji huyo wa Manchester United aliachwa katika kikosi cha Hodgson kutokana na majeruhi ya goti wakati Uingereza ilipofanikiwa kutoka nyuma na kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Ujerumani katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliofanyika jijini Berlin. Nyota Tottenham Hotspurs Dele Alli mwenye umri wa miaka 19 ndio alikuwa nyota wa mchezo na ushiriano wake na Harry Kane ndio uliochangia kwa kiasi kikubwa Uingereza kurejea mchezoni. Mbali na hao lakini moto alioonyesha mshambuliaji wa Leicester City Jamie Vardy nao umeongeza shinikizo katika nafasi ya Rooney kwenye kikosi cha kwanza cha nchi hiyo. Hata hivyo, Hodgson amempoza Rooney akisisitiza kuwa bado nahodha huyo yuko katika mipango yake kwani amekiongoza kikosi chake vyema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

No comments:

Post a Comment