Thursday, March 24, 2016

JABALI LA SOKA LA UHOLANZI NA BARCELONA LAFARIKI.

NGULI wa soka wa zamani wa Uholanzi na Barcelona, Johan Cruyff amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 68 kufuatia kusumbuliwa na maradhi ya saratani. Mchezaji huyo wa zamani wa Ajax Amsterdam na Barcelona alitangaza kusumbuliwa na maradhi hayo Octoba mwaka jana akieleza kuwa alitakiwa kufanyiwa upasuaji wa moyo. Katika taarifa iliyotumwa katika mtandao wake, imedai kuwa Cruyff alifariki dunia leo akiwa amezungukwa na familia yake hospitalini. Cruyff alijitengenezea jina akiwa na Ajax akishinda mataji manane ya ligi na klabu hiyo ktika vipindi viwili tofauti na kuanzisha falsafa yake katika soka ambayo ilikuja kujulikana kama Total Football. Akiwa chini ya kocha Rinus Michels, Cruyff pia alifanikiwa kutinga fainali ya Kombe la Dunia mwaka 1974 akiwa na Uholanzi watu wengi wakimtaja kama mchezaji bora kabisa wa taifa hilo kuwahi kutokea. Mbali na kupata mafanikio akiwa mchezaji, Cruyff pia alifanikiwa akiwa kocha na kufanikiwa kuingoza Barcelona kushinda mataji manne ya La Liga, Kombe la Washindi Ulay na Ligi ya Mabingwa Ulaya kuanzia mwaka 1988 mpaka 1996. Nguli huyo atakumbukwa kwa kuanzisha falsafa nyingine ya tiki-take ambayo imewapa umaarufu mkubwa Barcelona kwa kuitumia kwenye mfumo wao wa vijana ambao uliwaibua kina Xavi, Andres Iniesta pamoja na Lionel Messi.

No comments:

Post a Comment