MSHAMBULIAJI nyota wa Barcelona, Lionel Messi amekuwa mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kufunga mabao matatu au hat-trick dhidi ya APOEL Nicosia. Messi aliingia katika mchezo wa kundi F huko Cyprus akiwa amelingana kwa mabao 71 na mshambuliaji wa zamani wa Real Madrid Raul. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo ambao pia ulishuhudia Luis Suarez akifunga bao lake la kwanza toka sajiliwe, Messi mwenye umri wa miaka 27 amesema anajisikia furaha kuweka rekodi hiyo nzuri katika michuano muhimu kama hiyo. Messi aliendelea kudai kuwa pamoja na hilo lakini jambo muhimu kwake ni alama tatu walizopata na kuwapongeza wachezaji wenzake kwa kuonyesha soka safi. Hiyo inakuwa rekodi ya pili kubwa kwa Messi aliyoweka ndani ya siku nne, baada ya kuwa mfungaji bora la Liga kwa kufikisha mabao 253 kwa kufunga hat-trick nyingine katika mchezo dhidi ya Sevilla Jumamosi iliyopita. Nyota huyo wa kimataifa wa Argentina sasa anakuwa amefunga mabao 74 katika mechi 91 za michuano ya Ligi ya Mabingwa alizocheza wakati Raul yeye ana mabao 71 katika mechi 104 za michuano hiyo alizocheza.
No comments:
Post a Comment