KLABU kongwe jijini Instabul ya Galatasaray wanatarajia kumteua kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Uturuki Hamza Hamzaoglu kuwa meneja mpya wa klabu hiyo baada ya kutimuliwa kwa Muitaliano Cesare Prandelli. Klabu hiyo ilimtimua Prandelli baada ya kuitumikia chini ya nusu ya msimu kutokana na matokeo mabovu ambayo wamekuwa wakipata. Hamzaoglu amekuwa akiitumikia Uturuki chini ya kocha mkuu Fatih Terim toka mwaka 2013, na uamuzi wake huo umekuja baada ya kufanya mazungumzo na kocha huyo. Bodi ya klabu hiyo ilifikia uamuzi wa kumtimua Prandelli baada ya kutandikwa na Anderlecht kwa mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano usiku na kufuta matumaini yao ya kufuzu hatua ya mtoano. Prandelli alitua katika klabu hiyo Julai mwaka huu akichukua nafasi ya Muitaliano mwenzake Roberto Mancini na kupewa mkataba wa miaka miwili uliokuwa na thamani ya euro milioni 2.3.
No comments:
Post a Comment