Monday, June 27, 2016

COPA AMERICA 2016: BAADA YA KUSHINDWA FAINALI NNE, MESSI AAMUA KUTUNDIKA DARUGA ZAKE.



MSHABULIAJI nyota Lionel Messi ametangaza kustaafu soka la kimataifa baada ya kukosa mkwaju wa penati wakati Argentina iliposhindwa katika fainali yake nne kubwa katika kipindi cha miaka tisa. Akihojiwa mara baada ya kipigo hicho kutoka kwa Chile katika michuano ya Copa America, Messi mwenye umri wa miaka 29 amesema amefanya kila analoweza na ameona sio bahati yake hivyo ameamua kustaafu kuitumikia nchi yake. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa wamefanikiwa kufika katika fainali nne za mashindano makubwa na alikuwa akihitaji hilo kwa hamu kubwa lakini ameshindwa hivyo anaona inatosha ili aweze kuwapisha wengine. Akiwa na Barcelona, Messi amefanikiwa kunyakua mataji nane ya La Liga na manne ya Ligi ya Mabingwa ulaya lakini akiwa na Argentina amefanikiwa kutwaa medali ya dhahabu mwaka 2008 pekee. Argentina walitandikwa bao 1-0 katika fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2014 kabla ya kupoteza fainali mbili za Copa America kwa Chile zote zikiamuliwa na changamoto ya mikwaju ya penati. Messi pia alikuwepo katika kikosi cha Argentina kilichopoteza mchezo wa fainali ya michuano ya Copa America dhidi ya Brazil mwaka 2007. Katika mchezo huo uliochezwa mapema leo, timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana katika muda wa kawaida na ule wa nyongeza kabla ta Chile hawajashinda kwa penati 4-2.

No comments:

Post a Comment