Monday, June 20, 2016

AWEKA REKODI YA KUWA MCHEZAJI MWENYE UMRI MKUBWA ZAIDI KUFUNGA BAO JAPAN.

MCHEZAJI soka wa Japan, Kazuyoshi Miura amevunja rekodi yake mwenyewe ya kuwa mchezaji mzee zaidi kufunga bao katika ligi ya nchi hiyo. Miura alifunga bao katika dakika ya 22 ya mchezo wa ligi daraja la pili lakini timu yake ya Fc Yokohama ilifungwa mabao 2-1 na Fc Gifu katika mchezo huo. Mchezaji huyo amefunga bao hilo akiwa amefikisha umri wa miaka 49, miezi mitatu na siku 24, akivunja rekodi yake mwenyewe aliyoweka mwaka jana. Mshambuliaji huyo kwasasa amecheza misimu 31 ya soka baada ya kusaini mkataba mpya wa nyongeza Novemba mwaka jana. Miura amefunga mabao 55 katika mechi 89 alizoichezea Japan baada ya kuitwa katika kikosi hicho kwa mara ya kwanza mwaka 1990 lakini hakuwahi kushiriki fainali zozote za Kombe la Dunia. Anayeshikilia rekodi ya mchezaji mzee zaidi kufunga bao katika Ligi Kuu ya Japan maarufu kama J-League ni kocha wa zamani wa timu ya taifa ya nchi hiyo Zico ambaye alifunga bao akiwa na timu ya Kashima Antlers akiwa na umri wa miaka 41 mwaka 1994.

No comments:

Post a Comment