Sunday, June 19, 2016

RONALDO AWATAKA WACHEZAJI WENZAKE KUTOKATA TAMAA.

MSHAMBULIAJI nyota na nahodha wa kikosi cha timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo amesisitiza kuwa hawapaswi kukata tamaa ya kutinga hatua ya 16 bora pamoja na sare mbili walizopata katika mechi zao zilizopita. Kauli ya Ronaldo imekuja kufuatia sare ya bila kufungana walipata dhidi ya Austria huku nyota huyo akikosa penati. Pamoja na kuanza kwao taratibu Ronaldo amewataka wachezaji wenzake kutokukata tamaa kwani bado wana uwezo wa kutinga hatua ya mtoano. Ronaldo ambaye amefikia rekodi ya Luis Figo ya kucheza mechi nyingi za kimataifa, amesema matokeo dhidi ya Austria walikuwa hawayahitaji lakini huo ndio mchezo wa soka sio siku zote utaweza kushinda. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa walitengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini bahati haikuwa kwao hivyo jambo muhimu ni kuendelea kuamini kuwa wanaweza kufanya vizuri na kusonga mbele. Hungary ndio wanaoongoza kundi F wakiwa na alama nne, Iceland wanashikilia nafasi ya pili wakiwa na alama mbili, Ureno wa tatu wakiwa pia na alama mbili lakini wakitofautiana mabao na Austria ndio wanashikilia mkia kwenye hilo wakiwa na alama moja. Ureno wanatarajiwa kucheza na Hungary Jumanne ijayo jijini Lyon wakati Iceland wakipepetana na Austria siku hiyohiyo huko Stade de France.

No comments:

Post a Comment