KOCHA wa timu ya taifa ya Argentina, Gerardo Martino amesema Lionel Messi amekuwa akicheza kwa kiwango chake cha juu wakati wote wa michuano ya Copa America kama anavyokuwa katika klabu yake ya Barcelona. Argentina wanatarajiwa kukutana na mabingwa watetezi Chile baadae leo katika mchezo wa fainali ikiwa ni kama marudio ya fainali ya mwaka jana ambapo wenyeji Chile walishinda kwa changamoto ya mikwaju ya penati baada ya timu hizo kutoka sare ya bila kufungana huko Santiago. Messi alifanikiwa kufunga bao moja pekee katika michuano hiyo ya mwaka jana, lakini pamoja na majeruhi yaliyomfanya asicheze katika mechi ya kwanza ya michuano ya mwaka huu ambayo ni maalumu kusherekea miaka 100, tayari ameshafunga mabao matano na kusaidia mengine manne katika mechi tano alizocheza. Akihojiwa kuelekea katika mchezo huo mapema leo, Martino amesema Messi amekuwa katika kiwango bora kama anavyokuwa Barcelona na hilo limetokana na kucheza pamoja na wachezaji haohao kwa kipindi kirefu jambo ambalo linamfanya kujisikia vyema na furaha. Messi alifunga mabao manne katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014, yote akifunga katika hatua ya makundi na kuingoza nchi yake kutinga fainali ambapo walipoteza kwa Ujerumani katika dakika za nyongeza. Lakini aliondoka na tuzo ya mpira wa dhahabu akiwa mchezaji bora wa mashindano hayo yaliyofanyika nchini Brazil na pia alitajwa kama kikosi cha mashindano katika michuano ya Copa Amerika mwaka 2015.
No comments:
Post a Comment