SHIRIKISHO la Soka la Senegal, kimetoa orodha ya majina ya makocha 11 ambao wanawania nafasi ya kuinoa timu ya taifa ya nchi hiyo inayojulikana kama Simba wa Teranga. Aliyekuwa kocha wa timu hiyo Alain Giresse raia wa Ufaransa alijiuzulu nafasi hiyo Januari 29 mwaka huu baada ya kutolewa katika hatua ya makundi ya michuano ya Mataifa ya Afrika yaliyofanyika huko Guinea ya Ikweta. Makocha wa zamani wa Burkina Faso Paulo Duarte na Paul Put pamoja na Michel Dussuyer ambaye aliingoza Guinea katika michuano ya mwaka huu na Patric Neveu wote wametuma maombi yao. Wengine ni Jose Anigo, Frederic Antonetti, Luis Fernandez na Jean-Pierre Parin wote kutoka Ufaransa pamoja na Michel Pont kutoka Switzerland. Makocha wazawa waliotuma maombi yao ni pamoja na Amara Traore ambaye aliwahi kuiongoza Senegal kati ya mwaka 2009 na 2012, Aliou Cisse, Lamine Dieng na Oumar Diop. Shirikisho hilo limesema linategemea maombi zaidi kabla ya muda wa mwisho huku wakitarajia kutangaza jina la kocha mpya Machi mosi mwaka huu.
No comments:
Post a Comment