Thursday, February 19, 2015

UEFA CHAMPIONS LEAGUE: PORTO YANG'ANG'ANIWA NA BASEL, MADRID WAPETA.

MICHUANO ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliendelea jana kwa mechi mbili zingine kuchezwa ambapo mabingwa watetezi Real Madrid walikuwa wageni wa Schalke ya Ujerumani huku FC Basel ya Uswisi wenyewe wakiikaribisha FC Porto ya Ureno. Katika mchezo kati ya Basel na Porto ambao ulishuhudia mwamuzi Clattenburg akitoa kadi tisa za njano timu hizo zilitoka sare ya kufungana bao 1-1. Kwa upande wa Madrid wao kazi yao haikuwa ngumu sana kwani walifanikiwa kuibuka na ushindi mzuri wa mabao 2-0 dhidi ya Schalke huku mshambuliaji wake nyota Cristiano Ronaldo akimaliza ukame wa mabao kwa kufunga bao la kuongoza katika dakika ya 26 huku lingine likifungwa na Marcelo katika dakika ya 79. Kabla ya kwenda katika mechi za marudiano za michuano hiyo kutakuwa na mechi zingine za mkondo zitakazochezwa wiki ijayo ya Februari 24 na 25 ambapo mabingwa wa Italia Juventus watakuwa wenyeji wa Borussia Dortmund ya Italia na mabingwa wa Ligi Kuu Manchester City wakiwakaribisha Barcelona ya Hispania. Katika michezo itakayochezwa Februari 25 Arsenal ya uingereza watakuwa wenyeji wa Monaco ya Ufaransa huku Bayer Leverkusen ya Ujerumani wao wakipepetana na Atletico Madrid ya Hispania.

No comments:

Post a Comment