Wednesday, July 31, 2013

SPURS YAKUBALI KUANZA MAZUNGUMZO NA MADRID.

HATIMAYE klabu ya Tottenham Hotspurs imeanza mazungumzo na klabu ya Real Madrid juu ya mauzo ya euro milioni 115 ya mshambuliaji wake Gareth Bale baada ya viongozi wa klabu hiyo kushawishika kwamba nyota huyo ataondoka katika kipindi cha usajili wa majira ya kiangazi. Mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy alikuwa amekomaa katika kipindi chote toka dirisha la usajili lilipofunguliwa akidai kuwa hawana mpango wa kumuuza mchezaji huyo kwa gharama yoyote. Hata hivyo kampeni za Madrid za kutaka kumsajili nyota huyo zilionyesha kuzaa matunda siku chache zilizopita baada ya kumuonya mchezaji huyo na washauri wake kuwa aombe kuondoka hivi sasa au waachane naye kabisa. Onyo hilo la Madrid limeonyesha kuzaa matunda baada ya Bale kukutana binafsi na Levy na kumuhabarisha kuwa anataka kwenda zake kwa vigogo hao wa soka nchini Hispania. Hatua hiyo imepelekea Levy ambaye msimamo wake wa kutomuuza Bale ulikuwa ukiungwa mkono na mmiliki wake Joe Lewis, kufungua mazungumzo na Madrid ambapo anatarajiwa kukutana na rais wake Florentino Perez Agosti 6 mwaka huu jijini Florida.

No comments:

Post a Comment