Tuesday, July 18, 2017

LUKAKU AFUNGUA PAZIA LA MABAO UNITED, MOURINHO AMFAGILIA.

MSHAMBULIAJI Romelu Lukaku amefunga bao lake la kwanza akiwa Manchester United kufuatia ushindi wa mabao 2-1 waliopata katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Real Salt Lake uliofanyika huko Utah mapema leo Alfajiri. Lukaku ambaye amejiunga na United akitokea Everton kwa kitita cha paundi milioni 75 wiki iliyopita, alifunga bao hilo dakika ya 38 akimalizia pasi murua ya Henrikh Mkhitaryan. Nyota huyo wa kimataifa wa Ubelgiji mwenye umri wa miaka 24 pia alihusika katika bao la kusawazisha lililofungwa na Mkhitaryan dakika ya 29 baada ya Luis Silva kuifungia Salt Lake bao la kuongoza. Akizungumza na wanahabari kuhusiana na hilo, meneja wa United Jose Mourinho amesema bao hilo la Lukaku ni muhimu kwake na alishamwambia kabla ya mchezo huo kuwa anapenda kila kitu anachofanya. Ijumaa hii United inatarajiwa kuchuana na Manchester City kwenye mchezo mwingine wa kirafiki utakaofanyika jijini Houston.

No comments:

Post a Comment