Thursday, August 28, 2014

PLATINI AMGWAYA BLATTER, ABAINISHA KUWA HATAGOMBEA URAIS FIFA KATIKA UCHAGUZI WA MWAKANI.

RAIS wa Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA, Michel Platini amebainisha kuwa hana mpango wa kugombea nafasi ya urais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kwani anataka kutilia mkazo kibarua chake cha sasa kuliko kushindana na Sepp Blatter katika uchaguzi ujao. Mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa alikuwa akiaminika kuwa anafikiria kugombea nafasi nhiyo lakini alifafanua katika mkutano wa vyama 54 vya soka barani Ulaya uliofanyika huko Monte Carlo kuwa atabakia katika nafasi yake hiyo. Mjumbe wa kamati ya utendaji ya FIFA, Michel D’Hooge alikaririwa akidai kuwa ni ujumbe chanya uliotolewa na Platini na amefurahi kwani inamaanisha kuwa safari hii hakutakuwa na ushindani kati FIFA na UEFA. Platini amekuwa akimkosoa vikali Blatter kwa zaidi ya mara moja na mapema mwaka huu alieleza kuwa kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 78 amekwisha kama mtu sahihi wa kuiongoza FIFA. Blatter aliwahi kudai kuwa ataachia ngazi mwishoni mwa muhula wake huu wa nne lakini alibadili mawazo na uamuzi wake baadae na kuweka wazi kuwa atatetea tena kiti chake katika uchaguzi ujao. Blatter amekuwa akifanya kazi FIFA toka mwaka 1975 na alichaguliwa kwa mara ya kwanza kushika nafasi ya urais mwaka 1998.

No comments:

Post a Comment