KIUNGO wa zamani wa kimataifa wa Italia na klabu ya AC Milan, Gennaro Gattuso ametangaza kujiuzulu na kisha kubadili uamuzi wake huo baadae kuifundisha timu ya OFI Crete inayoshiriki Ligi Kuu nchini Ugiriki baada ya kuongoza mechi saba pekee. Gattuso mwenye umri wa miaka 36 alichukua mikoba ya kuinoa timu hiyo Juni mwaka huu lakini alitangaza kujiuzulu ghafla kufuatia kipigo walichoapata nyumbani cha mabao 3-2 kutoka kwa Asteras Tripolis. Katika mkutano wake na wanahabari, Gattuso amesema amekuwa akiifanya kazi hiyo kwa mapenzi na nguvu zake zote lakini hawezi kuwa pekee ambaye anapaswa kutatua matatizo ya timu hiyo kwani yeye sio rais na kazi yake inapaswa kuwa soka pekee. Lakini baada ya mazungumzo ya kina na uongozi wa klabu hiyo na jinsi mashabiki walivyomuunga mkono Gattuso aliamua kubadili uamuzi wake. Gattuso ambaye aliichezea Italia mechi 73 na kuisaidia kushinda Kombe la Dunia mwaka 2006 sambamba na kushinda mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Milan, alichukua nafasi ya Ricardo Sa Pinto kutoka Ureno ambaye aliingoza timu hiyo kumaliza katika nafasi ya sita katika msimamo wa ligi msimu uliopita.
No comments:
Post a Comment