Tuesday, October 28, 2014

ZIDANE AFUNGIWA MIEZI MITATU.

MCHEZAJI nguli wa zamani wa Ufaransa, Zinedine Zidane amefungiwa miezi mitatu leseni ya ukocha kwa kosa la kufundisha timu bila vyeti vilivyoruhusiwa. Shirikisho la Soka la Ufaransa lilimfungiwa kiungo huyo wa zamani kwa kuingoza timu ya Real Madrid ya Castilla kikiwa ni kikosi cha pili cha timu hiyo. Msaidizi wa Zidane katika timu hiyo Santiago Sanchez naye pia amefungiwa miezi mitatu. Katika taarifa yake klabu hiyo imebainisha kuwa hawatakubaliana na uamuzi huo na wamepanga kukata rufani na kudai kuwa Zidane ana kibali cha Shirikisho la Soka la Ufaransa cha kufanya kazi kama kocha mkuu. Zidane aliteuliwa kuwa kocha wa kikosi cha pili katika majira ya kiangazi baada ya kufanya kazi kama msaidizi wa Carlo Ancelotti msimu uliopita ambao Madrid walinyakuwa taji la 10 la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Zidane amewahi kuichezea Madrid kwa misimu mitano baada ya kujiunga nao akitokea Juventus kwa kitita cha paundi milioni 45 mwaka 2001 ada iliyovunja rekodi kwa wakati huo.

No comments:

Post a Comment