Monday, October 27, 2014

FAINALI YA KWANZA LIGI YA MABINGWA YAMALIZIKA KWA SARE.

MECHI ya mkondo wa kwanza ya fainali ya michuano ya Klabu ya Afrika baina ya timu za Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC na Entente Setif ya Algeria imechezwa jana kwa timu hizo kutoshana nguvu kwa kufungana mabao 2-2 jijini Kinshasa. Katika mchezo huo uliochezwa katika uwanja marufu wa Tata Raphael wageni Setif ndio walionza kufunga bao la kuongoza katika dakik ya 17 kupitia kwa Ndombe Mubele kabla ya bao hilon kusawazishwa na Chikito Lema Mabidi na kupelekea timu hizo kwenda mapumziko zikiwa sare. Katika kipindi cha pili Setif walicharuka tena na kupata bao katika dakika ya 58 kupitia kwa Akram Djahnit lakini Mabidi aliisawazishia Vita tena kwa shuti la umbali wa mita 30. Uwanja huo wa Tata Raphael ni maarufu kwani uliwahi kuchezwa kwa pambano la ngumi maarufu duniani lililopewa jina la Rumble ni the Jungle miaka 40 kati ya Mohammad Ali na George Foreman wote wa Marekani. Mubele sasa anaongoza katika orodha ya wafungaji katika michuano hiyo akiwa amefikisha mabao sita kuelekea mchezo wao marudiano utakaochezwa nchini Algeria, Novemba mosi mwaka huu. Mshindi katika fainali hiyo atajinyakulia kitita cha dola milioni 1.5 na nafasi ya kushiriki michuano ya Kombe la Dunia la Vilabu nchini Morocco Desemba mwaka huu.

No comments:

Post a Comment