KIUNGO wa zamani wa kimataifa wa Sweden na klabu ya Sheffield Wednesday, Klas Ingesson ambaye alikuwa sehemu muhimu ya kikosi cha timu yake ya taifa ambacho kilimaliza katika nafasi ya tatu katika Kombe la Dunia mwaka 1994 amefariki dunia kwa saratani akiwa na umri wa miaka 46. Akiwa mchezaji Ingesson alicheza katika vilabu kadhaa ikiwemo Gothenburg ya Sweden na Bolgona, Bari na Lecce zote za Italia kabla ya kuanza kuinoa timu ya Elfsborg ya nchini kwake. Sheffield Wednesday walituma salamu zao za rambirambi kwa mchezaji wao huyo wa zamani kupitia katika mtandao na kudai kuwa mawazo na fikra zao zipo pamoja na familia na marafiki wa Ingesson katika kipindi hiki kigumu. Ingesson aliwahi kuichezea Sweden mechi 57 huku akiiongoza vyema nchi yake kuitandika Bulgaria kwa mabao 4-0 na kuchukua nafasi ya tatu katika michuano ya Kombe la Dunia iliyofanyika nchini Marekani. Nyota huyo aligundulika kuwa na saratani katika mifupa mwaka 2009.
No comments:
Post a Comment