NGULI wa soka wa zamani wa Cameroon, Roger Milla amekosoa ombi la Morocco la kuahirisha michuano ya Mataifa ya Afrika-AFCON kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Ebola. Michuano hiyo inatarajiwa kufanyika kuanzia Januari 17 mwakani lakini Morocco wametaka kusogezwa mbele wakati serikali na taasisi za kiafya duniani kote wakihangaika kuzuia virusi hivyo kusambaa zaidi. Maofisa wa afya wa Morocco wameonya kuwa maelfu ya watu wanaotarajiwa kuhudhuria michuano hiyo ya wiki tatu wanaweza kuleta maambukizi ya ogonjwa huo katika nchi hiyo iliyopo kaskazini mwa bara la Afrika. Hata hivyo, Milla amesema anadhani Morocco wanajaribu kuficha ukweli halisi kuwa hawataki kuwa wenyeji wa michuano hiyo kwa kisingizio cha Ebola. Milla ambaye alikuwa shujaa wa Cameroon mwaka 1990 kwa kufunga bao akiwa na umri mkubwa zaidi wa miaka 40, aliendelea kudai kuwa amekuwa akifuatilia na kwa maoni yake anaona Morocco hawahofii Ebola bali wana ajenda yao ya siri ambayo hawataki kuiweka wazi. Nguli aliendelea kudai kuwa mpango wa Shirikisho la Soka la Afrika-CAF kutaka kuipeleka michuano hiyo mahali pengine hadhani kama wanatatua tatizo bali wanalihamisha. CAF inatarajiwa kukutana na maofisa wa Shirikisho la Soka la Morocco Novemba 2 jijini Algiers ili kuzungumzia suala hilo.
No comments:
Post a Comment