Wednesday, October 29, 2014

RONALDO KUPUMZIKA KOMBE LA MFALME.

MABINGWA watetezi Real Madrid wanatarajia kumpumzisha mfungaji wao kinara Cristiano Ronaldo sambamba na wachezaji kadhaa wa kikosi cha kwanza kwa ajili ya mchezo wa mkondo wa kwanza wa Kombe la Mfalme dhidi ya timu ya daraja la tatu ya Cornella. Ronaldo ambaye amefunga mabao 16 katika mechi nane za La Liga na matatu katika mechi tatu za Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu anatarajiwa kupumzishwa sambamba na golikipa Iker Casillas, mabeki wa kati Sergio Ramos na Pepe sambamba na viungo Toni Kross na Luka Modric. Katika taarifa yake kwa wanahabari meneja wa Carlo Ancelotti amesema nafasi ya Casillas itazibwa na Keylor Navas na Javier Hernandez ambaye alichukuliwa kwa mkopo kutoka Manchester United anatarajiwa kuanza katika safu ya ushambuliaji sambamba na Karim Benzema. Madrid waliichapa Barcelona mabao 2-1 na kushinda taji hilo msimu wa 2013-2014. Mchezo huo wa leo utaikutanisha klabu tajiri ambayo wastani wa mapato yake kwa mwaka ni zaidi euro milioni 600, dhidi ya klabu ambayo bajeti yake kwa msimu mmoja haizidi kiasi cha euro milioni moja. Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa katika Uwanja wa Espanyol kwasababu uwanja wa Cornella uliopo pembeni una uwezo wa kuingiza mashabiki 1,500 pekee.

No comments:

Post a Comment