Sunday, August 26, 2012

ROONEY NJE YA UWANJA WIKI NNE.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uingereza na klabu ya Manchester United, Wayne Rooney anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa muda wa mwezi mmoja kufuatia majeraha aliyopata wakati timu yake ikiigaragaza Fulham kwa mabao 3-2 katika Uwanja wa Old Traford jana. Rooney alitolewa katika dakika za mwisho za mchezo huo huku mguu wake ukiwa umejaa damu baada ya kujiparua katika kiatu cha mshambuliaji wa Fulham Hugo Rodallega wakati akijaribu kumzuia mchezaji huyo asipige mpira langoni mwao. Picha za luninga zilionyesha jinsi mchezaji huyo alivyojiparua katika mguu wake wa kulia na meneja wa United Sir Alex Ferguson alithibitisha kuwa mchezaji huyo atakuwa nje ya uwanja kwa kipindi hicho cha wiki nne. Kama Rooney hatapona haraka, anatarajiwa kukosa michezo mitatu ambayo timu yake itacheza na timu za Southampton, Wigan na Liverpool huku pia akikosa mchezo wa ufunguzi katika hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Mbali na michezo hiyo pia kocha wa timu ya taifa ya Uingereza inabidi atafute mbadala wa mchezaji huyo katika michezo miwili ya kufuzu michuano ya Kombe la Dunia dhidi ya Moldova na Ukraine mapema mwezi ujao.

No comments:

Post a Comment