Friday, August 24, 2012

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

MICHUANO YA KOMBE LA TAIFA 2012
Michuano ya Kombe la Taifa (Taifa Cup) inayoshirikisha kombaini za mikoa ya Tanzania Bara haitakuwepo mwaka huu kutokana na kukosekana kwa udhamini. Licha ya kukosekana kwa udhamini, awali tulifikiria kuendesha mashindano hayo kwa michango ya wanachama wetu (vyama vya mpira wa miguu vya mikoa) na Serikali za mikoa kugharamia timu zao. Lakini baadhi ya wanachama wetu na Serikali za mikoa walitushauri kuwa ni ngumu kuendesha mashindano hayo kwa sasa kutokana na shughuli za kitaifa zinazoendelea hivi sasa ikiwemo maandalizi ya sensa ya watu na makazi. Kwa mujibu wa Kalenda ya Matukio ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), mashindano ya Kombe la Taifa yalitakiwa kufanyika kuanzia Julai 23 hadi Agosti 6 mwaka huu. Michuano ya Kombe la Taifa msimu uliopita ilidhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager ambapo Mbeya iliibuka mabingwa katika fainali iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha.

WACHEZAJI 11 KUTOKA NJE WAPATA ITC
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa wachezaji 11 wa nje kati ya 14 walioombea usajili na klabu mbalimbali za Ligi Kuu. Wachezaji walioombewa usajili Yanga na tayari ITC zao zimepatikana ni Nizar Khalfan kutoka Vancouver Whitecaps ya Canada, Didier Kavumbagu (Atletico Olympic- Burundi) na Mbuyu Twite kutoka FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC). Kwa upande wa Simba ni Musa Mude (Sofapaka, Kenya) na Daniel Akuffor (Stella Abidjan, Ivory Coast) wakati Mtibwa Sugar ni Shabani Kisiga timu ya El Itihad ya Oman. Waliopata ITC kwa upande wa Kagera Sugar ni Wilfred Ojodale Ame na Benjamin Efe Ofuyah wote kutoka FC Abuja ya Nigeria. Wengine ni Deangelis Silva kutoka New Road ya Nepal kwenda Coastal Union, George Odhiambo kutoka Randers FC ya Denmark kwenda Mtibwa Sugar na Jerry Santo kutoka Tusker, Kenya kwenda Coastal Union. Wachezaji ambao wameombewa usajili na ITC zao bado hazijapatikana ni Salum Kinje na Pascal Ochieng wa AFC Leopards, Kenya kwenda Simba na Ayoub Hassan Isiko kutoka Bull FC, Uganda kwenda Mtibwa Sugar. Bado klabu ambazo hazijakamilisha usajili na kupata ITC zina fursa ya kufanya hivyo hadi Septemba 4 mwaka huu ambapo dirisha litafungwa. Pia TFF imetoa ITC kwa wachezaji wanane walioombewa kwenda kucheza mpira wa miguu katika nchi za Kenya na Msumbiji kutoka katika klabu mbalimbali za hapa nchini. Wachezaji hao na klabu wanazokwenda katika mabano ni Abdallah Ally Abdallah (CD Madchegde, Msumbiji), Almasi Khatib Mkinda (Ferroviario da Beira, Msumbiji), David Naftali (Bandari, Kenya) na Hassan Hassan Mustafa (CD Madchegde, Msumbiji). Wengine ni Meshack Abel (Bandari, Mombasa), Mohamed Banka (Bandari, Kenya), Thobias Davis Silas (CD Madchegde, Msumbiji) na Thomas Maurice (Bandari, Kenya).

VIPIMO VYA TIBA KWA WACHEZAJI
Klabu zote zilizowasilisha Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) maombi ya usajili kwa wachezaji wao zinatakiwa pia kuwasilisha nakala za hati zao za vipimo vya afya (medical certificate) kwa mujibu wa kanuni za usajili.

No comments:

Post a Comment