Thursday, August 23, 2012

CHELSEA YAKATAA PAUNDI MILIONI 30 ZA MAN CITY KWA AJILI YA LUIZ.

KLABU ya soka ya Chelsea imekataa kitita cha paundi milioni 30 kutoka kwa klabu ya Manchester City ili wawauzie beki wao David Luiz. Meneja wa City Roberto Mancini alikuwa akihaha kutafuta beki wa kuziba pengo la Micah Richards ambaye ni majeruhi na atakuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki 10. Luiz hakuwemo katika kikosi cha Chelsea ambacho kilishinda mabao 4-2 dhidi ya Reading wakati pande zote zikifanya mazungumza kuhusu mchezaji huyo ingawa hata hivyo beki huyo wa kimataifa wa Brazil alidai katika mtandao wa kijamii wa twitter kwamba alikuwa na majeraha ya goti. Ujumbe huo aliotuma twitter ulionyesha kumkera meneja wa Chelsea Roberto Di Matteo na kudai kuwa ataangalia uwezekano wa kuzuia masuala mengine kwa wachezaji wake wasiyaweke wazi katika mitandao hiyo. Luiz mwenye umri wa miaka 25 aliwasili Stamford Bridge kwa ada ya paundi milioni 21 kutoka klabu ya Benfica ya Ureno na toka kipindi hicho amekuwa kipenzi cha mashabiki wa klabu hiyo kutokana na umahiri wake wa kukaba na kushambulia alionao.

No comments:

Post a Comment