Monday, August 27, 2012

MOURINHO AWAPONDA WACHEZAJI WAKE KUCHEZA HOVYO.

MENEJA wa klabu ya Real Madrid Jose Mourinho amewalaumu wachezaji wake kwa kushindwa kucheza vizuri na kupelekea timu hiyo kuchapwa mabao 2-1 dhidi ya majirani zao Getafe katika mchezo wa Ligi Kuu nchini Hispania maarufu kama La Liga. Kipigo hicho kilimaliza ubabe wa Madrid ambao ni mabingwa watetezi kutofungwa katika michezo 24 ya ligi iliyopita huku pia ukiwa ni mchezo wa kwanza kupoteza katika kipindi cha miaka mitano katika La Liga baada ya kuongoza katika kipindi cha kwanza. Akihojiwa Mourinho amesema kuwa wachezaji wake hawakucheza mchezo mzuri kabisa na kwamba walistahili kufungwa katika mchezo lakini alikataa kumlaumu mchezaji mmoja mmoja na kusema kuwa wana kazi kubwa ya kufanya ili kurejea katika kiwango chao. Madrid ambao katika mchezo wa kwanza wa La Liga dhidi ya Valencia walitoka sare ya bao 1-1, kipigo hicho kinawaacha nyuma ya alama tano mbele mahasimu wao Barcelona ambao wameshinda katika michezo yao yote miwili. Mara ya mwisho Madrid kupoteza michezo yake miwili ya kwanza ilikuwa msimu wa mwaka 2001-2002 ambapo walimaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa La Liga na kupoteza mchezo wa fainali wa Kombe la Mfalme kwa Deportivo Coruna lakini walifanikiwa kushinda Kombe la Ligi ya mabingwa Ulaya wakiifunga Bayer Liverkusen katika mchezo wa fainali.

No comments:

Post a Comment