Tuesday, August 28, 2012

MADRID TUMBO JOTO MCHEZO WA KESHO DHIDI YA BARCELONA.

KLABU ya Real Madrid inatarajiwa kuikaribisha Barcelona katika mchezo wa pili wa Super Cup wakitambua kwamba wanahitaji ushindi ili kushinda taji lao la kwanza msimu huu. Kama klabu hiyo ikishindwa kuibuka kidedea katika mchezo huo itakuwa ni pigo kubwa katika kampeni yao ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu nchini Hispania maarufu kama La Liga baada ya kushindwa kupata ushindi katika michezo yao mitatu iliyotangulia. Mbali na kufungwa katika mchezo wao wa kwanza wa Super Cup na Barcelona kwa mabao 3-2 katika Uwanja wa Nou Camp, Madrid pia walipoteza mchezo wa La Liga dhidi ya Getafe kwa kufungwa mabao 2-1 na kuwapa nafasi mahasimu wao hao kuwaacha kwa alama tano wakiwa wameshinda michezo yao yote miwili. Meneja wa Madrid Jose Mourinho aliponda kikosi chake kwa mchezo waliocheza wakati akikataa kulaumu waamuzi wa mchezo huo kama alivyofanya katika mchezo dhidi ya Barcelona ambapo alidai bao la kwanza la timu hiyo lilikuwa la kuotea. Barcelona nao ambao msimu huu wameonekana kuanza vyema tofauti na msimu uliopita nao watakuwa wakisaka taji lao la kwanza msimu huu huku wakimkosa beki wao mahiri Carles Puyol ambaye aliumia katika mchezo wa Jumapili.

No comments:

Post a Comment