Friday, November 29, 2013

SIJUTI KUHAMIA MADRID - BALE.

WINGA mahiri Gareth Bale anafikiri kuwa Real Madrid ni klabu kubwa ulimwenguni na amedhamiria kushinda mataji akiwa hapo katika miaka mingi ijayo. Nyota huyo wa kimataifa wa Wales alijiunga na Madrid akitokea klabu ya Tottenham Hotspurs katika kipindi cha usajili majira ya kiangazi kwa ada iliyovunja rekodi ya euro milioni 100 na amesisitiza kuwa hajuti kuhamia Santiago Bernabeu. Bale aliuambia mtandao wa klabu hiyo kuwa kwa mawazo yake anadhani klabu hiyo ni bora duniani, wana wachezaji bora na uwanja mzuri huku kila kitu hapo kikiwa sawa. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa anataka kufanya kila awezalo ili kuisaidia timu na kushinda mataji ili kumuonyesha kila mtu kwamba Madrid ni klabu kubwa. Bale mwenye umri wa miaka 24 pia alimpongeza nyota mwenzake Cristiano Ronaldo na kudai kuwa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ureno yuko katika ligi yake ya kipekee. Amesema anadhani Ronaldo ni mchezaji bora duniani na ameonyesha hilo msimu huu tena akiwa chini ya shinikizo kama ilivyokuwa katika mchezo wa mtoano kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Sweden.

No comments:

Post a Comment