Thursday, November 28, 2013

NGULI WA ZAMANI WA ARSENAL ALAZWA KWA MARADHI YA SARATANI.

BEKI na kocha msaidizi wa zamani wa klabu ya Arsenal, Pat Rice ambaye aliitumikia timu hiyo ya Ligi Kuu nchini Uingereza kwa miaka 44 amelazwa hospitali kutokana na matatizo ya saratani. Rice, aliyewahi kuwa meneja wa muda wa Arsenal, alijiunga na klabu hiyo mwaka 1964 kabla ya kustaafu mwaka uliopita akiwa msaidizi wa kocha Arsene Wenger. Akihojiwa na mtandao wa Daily Mail msemaji wa Arsenal, amesema kila mtu katika klabu hiyo anamtakia heri Rice huku mawazo na fikra zao zikiwa karibu na familia yake katika kipindi hiki kigumu wanachopitia. Rice mwenye umri wa miaka 64 amecheza mechi 528 katika misimu 14 aliyochezea Arsenal baada ya kujiunga na kikosi cha vijana kilichoshinda Kombe la FA mwaka 1971. Baada ya kustaafu soka akiwa katika klabu ya Watford, Rice alijiunga na Arsenal tena akiwa kama kocha wa vijana mwaka 1984 kabla ya kuongeza ujuzi na kupanda cheo mpaka kuwa msaidizi wa Wenger na kushinda vikombe saba wakiwa wote.

No comments:

Post a Comment