TIMU ya mpira wa kikapu ya Cleveland Cavaliers imefanikiwa kutinga hatua ya fainali za NBA kwa mara ya tatu mfululizo baada ya kuichabanga Boston Celtics kwa vikapu 135-102. Sasa Cavaliers watakutana tena kwa mara tatu mfululizo na mabingwa wa Ukanda wa Magharibi Golden State Warriors katika fainali hizo. Kyrie Irving na LeBrone James kwa pamoja wamefunga alama 79 katika mchezo huo uliofanyika katika Uwanja wa TD Gardens jijini Boston na kutwaa ubingwa wa Kanda Mashariki kwa kushinda 4-1 kati ya mechi saba zilizotakiwa kuchezwa. James mwenye umri wa miaka 32, alifanikiwa kuipita rekodi ya nguli wa Chicago Bulls Michael Jordan ya mfungaji kinara wa wakati wote kwenye mechi za mtoano. Jordan aliweka rekodi ya kufunga alama 5,987 katika mechi 179, rekodi ambayo imedumu kwa miaka 19 mpaka James alipoivuka kwa kufunga alama 5,995 katika mechi 212 za mtoano alizocheza. Mechi ya kwanza ya fainali kati ya Cavaliers na Warriors inatarajiwa kuchezwa Juni mosi mwaka huu katika Uwanja wa Oracle Arena jijini Oakland.
No comments:
Post a Comment