KLABU ya Sevilla imetangaza kufikia makubaliano na Chama cha Soka cha Argentina-AFA ili meneja wake Jorge Sampaoli aende kuwa kocha wa timu ya taifa ya nchi hiyo. Sampaoli alijiunga na Sevilla kabla ya kuanza kwa msimu huu na kuwaongoza kushika nafasi ya nne katika msimamo wa La Liga, lakini mwishoni mwa kampeni kulizuka tetesi zilizomuhusisha kwenda kuinoa Argentina baada ya Edgardo Bauza kutimuliwa. Mwishoni mwa wiki iliyopita kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Chile alifafanua kuwa kuiongoza Argentina ni ndoto zake za kipindi kirefu na kwamba AFA inatakiwa kuzungumza na Sevilla kama wanamuhitaji. Katika taarifa yao iliyotumwa katika mtandao, Sevilla walithibitisha makubaliano baina yao kufikiwa na pande hizo mbili zitasaini makubaliano hayo Juni mosi mwaka huu. Kibarua cha kwanza cha Sampaoli kitakuwa mechi mbili za kirafiki ambazo Argentina inatarajiwa kucheza dhidi ya Brazil ,a Singapore mwezi ujao.
No comments:
Post a Comment