Tuesday, August 30, 2016

AYEW, GYAN WAJITOLEA KUISAIDIA BLACK STARS KUFUATIA UKATA ULIYOIKUMBA.

MSUGUANO kati ya Wizara ya Michezo ya Ghana na Shirikisho la Soka la nchi hiyo-GFA umechukua sura mpya kufuatia wachezaji wa kikosi cha kwanza kuambiwa kujilipia nauli zao wenyewe. Kuelekea mchezo wao wa mwisho wa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika Jumamosi hii, waziri wa michezo Nii Lante Vanderpuye ameiambia GFA kuwa hakutakuwa na fedha kwa ajili ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ambao wameitwa katika kikosi hicho cha Black Stars. Hatua hiyo imekuja kwa madai kuwa timu hiyo tayari imeshafuzu michuano hiyo itakayofanyika nchini Gabon mwaka 2017, hivyo wanaona ni upotevu wa fedha kuwasafirisha wachezaji kutoka Ulaya na kwingineko. Kutokana na hilo nahodha msaidizi wa Black Stars, Andre Ayew amejitolea kununua tiketi kwa baadhi ya wachezaji 21 kutoka nje walioitwa katika kikosi hicho kinachonolewa na Avram Grant kwa ajili ya mchezo huo dhidi ya Rwanda Septemba 3. Naye nahodha wa timu hiyo Asamoah Gyan pia atachangia chochote kwa kutoa baadhi ya tiketi kwa ajili ya wachezaji ambao hawataweza kumudu kununua tiketi.

No comments:

Post a Comment