Monday, August 22, 2016

OLIMPIKI YAMALIZIKA MAREKANI WAKIIBUKA WABABE.

MICHUANO ya Olimpiki imemalizika rasmi jijini Rio de Janeiro kwa sherehe kabambe ya kufunga na kuwakabidhi rasmi wenyeji wa michuano hiyo mwaka 2020 jiji la Tokyo. Sherehe hizo zilizopambwa na mambo mbalimbali ya tamaduni za watu wa Brazil zilidumu kwa muda wa saa tatu katika Uwanja wa Maracana kabla ya mwenge wa Olimpiki kukabidhiwa kwa wenyeji wajao Tokyo. Ofisa mkuu wa Kamati ya Kimataifa wa Olimpiki-IOC, Thomas Bach ameisifia Brazil kwa maandalizi mazuri ya michuano hiyo iliyochukua muda wa siku 16 kabla ya kutia nanga mapema leo alfajiri. Michuano hiyo ya 31 ilishirikisha jumla ya wanariadha 11,303 kutoka mataifa 206 na timu ya wakimbizi huku kukiwa na michezo 26 iliyokuw aikishindaniwa. Katika michuano ya mwaka huu Marekani ndio wameibuka wababe kwa kuzoa jumla ya medali 121, 46 zikiwa za dhahabu, 37 za fedha na 38 za shaba, wakifuatiwa na Uingereza waliozoa medali 67, 27 za dhahabu, 23 za fedha na 17 za shaba. Wengine wanaofuatia ni China waliobeba medali 70, 26 za dhahabu, 18 za fedha na 26 za shaba, Urusi wao wako nafasi ya nne wakiwa na medali 56, dhahabu 19, fedha 18 na shaba 19, Tano bora inafungwa na Ujerumani wlaiozoa medali 42, dhahabu 17, fedha 10 na shaba 15. Kwa upande wa Afrika, Kenya ndio wlaiofanikiwa zaidi kwa kuzoa medali 13, sita za dhababu, sita zingine za fedha na moja ya shaba, wakifuatiwa na Afrika Kusini waliochukua medali 10, mbili za dhahabu, sita za fedha na mbili zingine za shaba.

No comments:

Post a Comment