Sunday, June 22, 2014

KOMBE LA DUNIA 2014: VAN GAAL AILALAMIKIA FIFA KWA UPENDELEO.

KOCHA wa timu ya taifa ya Uholanzi, Louis van Gaal amelikosoa Shirikisho la Soka la Dunia-FIFA kwa kushindwa kutoa usawa kwa kuwalazimisha kucheza mchezo wao wa mwisho wa kundi B kabla ya kujua mpinzani watakaekutana naye katika hatua inayofuata ya timu 16 bora. Uholanzi tayari wameshafuzu hatua hiyo ya mtoano kufuatia ushindi wao dhidi ya Hispania na Australia ambapo wanatarajia kuchuana na Chile katika mchezo wao wa leo utakaochezwa saa moja usiku kwa saa za hapa wakitegemea kuchukua uongozi wa kundi lao. Mpinzani wao watakayekutana naye hatua inayofuata atatoka katika kundi A, ambapo Brazil, Croatia na Mexico wanafukuzia nafasi ya kufuzu mechi ambazo zitachezwa kwa pamoja saa tano usiku. Kupangwa kwa mechi za kundi A kuchezwa baada ya mechi za kundi B kunaonekana kutompendeza Van Gaal ambaye amedai anaona kama wenyeji wao wanapendelewa. Van Gaal amesema katika kila mechi FIFA wanaonyesha mabango ya kutaka usawa katika mchezo huo wa soka lakini kwa jinsi wanafanya kwa kuwapendelea wenyeji katika ratiba haoni usawa wowote. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa watakachofanya wao na kuzingatia ushindi katika mchezo wao dhidi ya Chile hadhani kama hilo litaathiriwa kwasababu Brazil wanacheza baada yao, wanachotegemea ni kuwa watakuwa wanamichezo.

No comments:

Post a Comment