BEKI wa zamani wa klabu ya Manchester United, Rio Ferdinand amekubali dili la kusajiliwa katika klabu ya Queens Park Rangers-QPR ambao wamepanda daraja msimu huu. Beki huyo mwenye umri wa miaka 35 ameshawishika kupunguziwa mshahara wake baada ya kusikia mipango ya Harry Redknapp ya jinsi gani anaweza kuisaidia klabu hiyo yenye maskani yake jijini London kujiimarisha katika Ligi Kuu. Inaaminika kuwa mshahara wa nyota huyo umepunguzwa mara tatu ya ule wa paundi 200,000 kwa wiki aliokuwa akiupata Manchester United huku pia akikataa ofa ya kufanya kazi katika vyombo vya habari ambapo BT na BBC walikuwa wakitaka kumuajiri. Usajili huo wa Ferdinand unatarajiwa kuthibitishwa na klabu hiyo siku chache zijazo. Kwasasa Ferdinand ambaye anafanya kazi na BBC nchini Brazil, ni mchezaji huru baada ya kuachwa na United kufuatia miaka 12 aliyoitumikia. Redknapp mwenye umri wa miaka 67 ndiye aliyempa nafasi ya kucheza Ferdinand wakati akiwa West Ham United mwaka 1996 kuja kuwa mmoja wa mabeki ghali zaidi duniani wakati akihamia Leeds kwa paundi milioni 18 miaka mitano baadae.
No comments:
Post a Comment