Tuesday, June 24, 2014

KOMBE LA DUNIA 2014: NEYMAR NI MUHIMU KWETU KAMA ILIVYO KWA MESSI ARGENTINA.

KOCHA wa timu ya taifa ya Brazil, Luiz Felipe Scolari amekiri Neymar ni mchezaji muhimu katika kikosi chake kama ilivyo kwa Lionel Messi katika kikosi cha Argentina baada ya kufunga mabao mawili kwenye ushindi wa mabao 4-1 waliopata kutoka kwa Cameroon. Nyota huyo wa Barcelona aliifungia Brazil bao la kuongoza katika dakika ya 17 akimalizia krosi ya chini iiyopigwa na Luiz Gustavo na kufunga bao lake la nne katika michuano hiyo kwa juhudi binafsi baadae katika kipindi cha kwanza. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo, Scolari alikiri kuwa Brazil inamtegemea Neymar kama ilivyo kwa Argentina na Messi. Scolari amesema wachezaji hao wawili ni tofauti na wanaweza kubadilisha matokeo katika timu zao wakati ambapo wanahitajika kufanya hivyo. Brazil imefanikiwa kuikwepa Uholanzi katika hatua ya timu 16 bora na sasa watachuana na Chile ambao wote wanatoka bara moja la Amerika Kusini lakini Scolari amesema kama angeambiwa achague basi angechagua timu nyingine. Scolari aliendelea kudai kuwa ni ngumu kucheza na mpinzani anayetoka Amerika ya Kusini kwasababu Chile wana wachezaji wengi wenye uwezo na wanacheza kwa umoja.

No comments:

Post a Comment