KIKOSI cha timu ya taifa ya Nigeria kimegoma kufanya mazoezi jana kufuatia kutoelewana juu ya posho zao za kuvuka hatua ya timu 16 bora katika michuano ya Kombe la Dunia inayoendelea nchini Brazil. Wachezaji wa timu hiyo waliomba mkutano na viongozi ambapo walitaka sehemu ya pesa zao ambazo zitatolewa na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kwa kuvuka hatua ya pili walipwe na Shirikisho lao la Soka la Nigeria. Kutokana na FIFA kuchelewa kutoa fedha hizo za bakshishi wachezaji wamesema shirikisho lao la soka linapaswa kuwalipa kabla ya hawajacheza mchezo wao dhidi ya Ufaransa Jumatatu. Wachezaji hao wameamua kufanya hivyo kwani wanajua wakitolewa katika michuano hiyo Jumatatu, itakuwa ngumu kupata fedha zao kutoka NFF kama ilivyokuwa katika michuano ya mwaka 2010. Migogoro ya fedha kwa timu za Afrika katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka huu imekuwa suala la kawaida hatua ambayo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa timu kukosa ari ya kujituma kutokana na kukosa haki zao. Timu za Cameroon na Ghana ambazo tayari zimeenguliwa katika michuano hiyo nazo zilikumbwa na migogoro kama hiyo ambayo ilipelekea wachezaji wa Cameroon kugoma kupanda ndege mpaka wapewe posho zao huku rais wa Ghana akilazimika kusafirisha fedha za ya dola milioni tatu kwa ndege ili kuzima mgomo uliotaka kutokea.
No comments:
Post a Comment