MAKAMU wa rais wa Shirikisho la Soka la Afrika-CAF, Seketu Patel amejitoa kutoka katika kinyang’anyiro cha kugombea nafasi mbili za Afrika katika Baraza la Shirikisho la Soka Duniani-FIFA. Hatua hiyo inafanya kubaki na wagombea watano katika uchaguzi huo ambao unatarajiwa kuteka sehemu kubwa ya Mkutano Mkuu Maalumu wa CAF utakaofanyika jijini Cairo kesho. CAF ilithibitisha taarifa hizo huku Patel mwenyewe akishindwa kutoa sababu zozote za kujitoa kwake kwenye kinyang’anyiro hicho. Rais wa Chama cha Soka cha Sudan Kusini, Chabur Goc Alei naye alijitoa katika kinyang’anyiro hicho wiki iliyopita. Hatua hiyo sasa inamuacha makamu wa pili wa rais wa CAF Almamy Kabele Camara kutoka Guinea kuwa mgombea mwenye hadhi ya juu zaidi katika mbio hizo na mmoja kati ya wanaopigiwa upatu wa kukwaa nafasi mojawapo pamoja na mjumbe wa kamati ya utendaji ambaye pia ni raia wa Chama cha Soka cha Ghana Kwesi Nyantakyi. Wagombea wengine katika uchaguzi huo ni Ahmad wa Madagascar ambaye hutumia jina moja pekee katika utambulisho wake, Hamidou Djibrilla wa Niger na rais wa Chama cha Soka cha Senegal Augustin Senghor.
No comments:
Post a Comment