RAIS wa Olympique Lyon, Jean-Michel Aulas amedai meneja Bruno Genesio na benchi lake la ufundi ndio walichukua uamuzi wa kumsajili Jean-Philippe Mateta badala ya Emmanuel Adebayor. Adebayor ambaye ni mchezaji huru alikuwa akitegemewa kujiunga na klabu hiyo ya Ligue 1 wiki iliyopita lakini dili hilo halikukamilika kama ilivyotarajiwa. Lyon ilieleza sababu za kumuacha mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 32 kuwa ni kukosekana kwake katika michuano ya Mataifa ya Afrika pamoja na kutoweza kushiriki hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Akihojiwa kuhusiana na suala hilo Aulas amesema Mateta mwenye umri wa miaka 19 ambaye amechukuliwa kutoka Chateauroux, alionyesha ni mtu sahihi kusajiliwa kuliko mkataba wa kipindi kifupi ambao angepewa Adebayor. Aulas amesema kutokana na kuumia kwa Alexandre Lacazette walikuwa wakitafuta mchezaji wa safu ya ushambuliaji ili kuziba nafasi hiyo na walikuwa na machaguo mengi kabla ya kocha na benchi lake kuamua kumchukua Mateta.
No comments:
Post a Comment