Thursday, February 21, 2013

BODI KUMHAKIKISHIA WENGER NAFASI YAKE.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger anatarajiwa kuhakikishiwa nafasi yake katika kikao cha bodi kitakachokutana pamoja na mmiliki wa klabu hiyo Stan Kroenke baadae leo. Klabu hiyo ilithibitisha katika mtandao wake kuwa Wenger atakutana na Kroenke ambaye aliwasili jijini London kuangalia mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ambao Arsenal ilichapwa kwa mabao 3-1 na Bayern Munich, baada ya muda wa mazoezi. Arsenal sasa inapigana ili isipate aibu nyingine ya kufungwa huko jijini Munich katika mchezo wa marudiano utakaochezwa Machi 13 na kuhakikisha inamaliza katika nafasi nne za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu nchini Uingereza. Wenger anakabiliwa na kibarua kingine kigumu Jumamosi wakati timu hiyo itakapoikaribisha Aston Villa katika mchezo wa ligi huku akikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mashabiki wa klabu hiyo wanaomtaka aondoke baada ya kukosa vikombe kwa kipindi cha miaka nane.

No comments:

Post a Comment