Monday, February 18, 2013

WAFANYAKAZI MARICANA WATISHIA KUGOMA TENA.

WAFANYAKAZI wanaofanya shughuli za ujenzi katika Uwanja wa Maracana nchini Brazil wametishia kugoma na kuwapa changamoto mpya waandaaji wa Kombe la Dunia ambao wanakimbizana na muda ili kumaliza uwanja huo kwa wakati. Wafanyakazi hao ambao wanadai nyongeza ya mshahara, vocha za chakula na bima binafsi ya afya kwa familia zao walisimama kufanya kazi kwa siku moja na kutishia kugoma kabisa kuanzia wiki ijayo. Uwanja huo maarufu ambao ulitumika katika baadhi mechi kwenye michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1950, unafanyiwa ukarabati kwa ajili ya kutumika katika michuano ya Kombe la Shirikisho na Kombe la Dunia mwakani ambapo utatumia kiasi cha dola milioni 458. Uwanja huo ulipangwa kufunguliwa rasmi katika mchezowa kimataifa wa kirafiki kati ya Brazil na Uingereza June 2 mwaka huu na kuandaa mchezo wa kwanza wa ushindani kati ya Mexico na Italy June 16 kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho. Ujenzi wa uwanja huo tayari umevuka muda wake ambapo ulitakiwa kuisha Desemba mwaka jana na sasa wameamua kufanya kazi bila kupumzika huku wafanyakazi wakipishana mara tatu kwa siku ili wamalize kabla ya tarehe ya mwisho ambayo ni April 15.

No comments:

Post a Comment