MFANYABIASHARA na mwanasiasa wa Afrika Kusini, Tokyo Sexwale amesisitiza leo kuwa ataendelea na mbio za kuwania urais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA pamoja na wasiwasi uliopo katika kampeni zake. Akizungumza na wanahabari katika kikao chake maalumu na maofisa wa mashirikisho ya nchi za Amerika Kaskazini na Kusini jijini Zurich, Sexwale amesema pamoja na magumu yote anayopitia lakini bado ataendelea kupambana. Sexwale mwenye umri wa miaka 62 aliendelea kudai kuwa wamekwenda pale kwa ajili ya FIFA kwani shirikisho hilo ni kama nyumba iliyobomoka hivyo inahitaji mtu sahihi wa kuirekebisha. Sexwale anachuana na Sheikh Salman bin Ibrahim Al-Khalifa wa Bahrain, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA Gianni Infantino, makamu wa zamani wa rais wa FIFA Prince Ali bin al-Husein na Ofisa wa amani wa FIFA Jerome Champagne. Uchaguzi wa shirikisho hilo ambao utashirikisha wajumbe 207 unatarajiwa kufanyika kesho huko Zurich, Uswisi.
No comments:
Post a Comment