Wednesday, February 24, 2016

WENGER ATUPA TAULO, ADAI BARCELONA WAMEFUZU KWA ASILIMIA 95.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amedai kuwa Barcelona wamefuzu kufika robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa asilimia 95 baada ya kikosi chake kukubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa mabingwa hao wa Hispania. Wenger raia wa Ufaransa ameilaumu safu yake ya ushambuliaji kwa kushindwa kutumia vyema nafasi walizopata katika mchezo huo wa mkondo wa kwanza uliofanyika katika Uwanja wa Emirates. Nyota wa Arsenal Alex Oxlade-Chamberlain na Olivier Giroud walikosa nafasi za wazi kabla ya Barcelona hawajafunga bao la kuongoza kupitia kwa nyota wake Lionel Messi. Akihojiwa Wenger amesema kwa jinsi walivyokuwa wakitumia nafasi za mwisho ni tatizo hivyo wanapaswa kujirekebisha haraka kabla ya mchezo wa maruadiano. Meneja huyo aliendelea kudai kuwa kimahesabu Barcelona wameshafuzu kwa asilimia 95 lakini wanataka kwenda Camp Nou kucheza hivyo anaamini wanaweza kupata nafasi hata hiyo kiduchu iliyobakia.

No comments:

Post a Comment