WINGA wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa na klabu ya Arsenal, Robert Pires ametangaza rasmi kutundika daruga zake akiwa na umri wa miaka 42. Pires pia amecheza katika klabu za Metz, Marseille, Villarreal na Aston Villa kabla ya kwenda kumalizia soka lake katika klabu inayoshiriki Ligi Kuu ya India, Goa ambako aliondoka Machi mwaka jana. Mkongwe huyo aliliambia jarida la L’Equipe kuwa kwa umri aliofikia anadhani wakati wa yeye kuacha kucheza soka umefika ili aweze kupisha nafasi kwa vijana wanaochipukia. Akiwa na kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa, Pires alifanikiwa kushinda taji la Kombe la Dunia mwaka 1998, Euro mwaka 2000 na mataji mawili ya Kombe la Shirikisho kabla ya kuacha mechi za kimataifa mwaka 2004. Kwa upande wa vilabu, Pires alifanikiwa kucheza kwa mafanikio akiwa na Arsenal kuanzia mwaka 2000 mpaka 2006 na kushinda mataji mawili ya Ligi Kuu ikiwemo msimu wa 2003-2004 ambao walishinda taji hilo bila kufungwa mechi yeyote.
No comments:
Post a Comment