MSHAMBULIAJI nyota wa Borussia Dortmund, Pierre-Emerick Aubameyang amebainisha kuwa alikaribia kujiunga na Newcastle United miaka mitatu iliyopita lakini alibadili uamuzi na kuamua kwenda Ujerumani. Nyota huyo wa kimataifa wa Gabon sasa ni mmoja kati ya washambuliaji hatari barani Ulaya akiwa amefunga mabao 21 katika Bundesliga msimu huu huku akiripotiwa kuwindwa na klabu za Manchester United na Chelsea kwa kitita cha paundi milioni 70. Mwaka 2013 klabu ya zamani ya mshambuliaji huyo Saint-Etienne ya Ufaransa ilimlazimisha kujiunga na Newcastle lakini aliwakatalia na kuamua kwenda Dortmund pamoja na dau kubwa alilowekewa na klabu hiyo. Akihojiwa Aubameyang amesema alipata ofa kutoka Qatar ambayo ingemuwezesha kukunja kitita cha euro milioni 10 kwa mwaka lakini aliamua kubakia Saint-Etienne ambako alikuwa akipata euro 70,000 kwa mwezi akifahamu kuwa kutokana na ubora wake atakuja kupata fedha nyingi zaidi baadae. Nyota huyo anaendelea kudai kuwa msimu uliofuata Saint-Etienne ilitaka kumuuza Newcastle lakini aliamua kuichagua Dortmund kwakuwa baba yake aliona mbinu za Jurgen Klopp zingemfaa kwenye klabu hiyo pamoja na mshahara mdogo atakaopokea.
No comments:
Post a Comment