MENEJA mpya wa klabu ya Manchester United, Louis van Gaal, amekiri kuwa bado anatafuta beki mmoja kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu. United tayari imeshawasajili Luke Shaw na Ander Herrera katika kipindi hiki cha kiangazi wakati Van Gaal naye akiwapa nafasi chipukizi Reece James, Michale Keane na Tyler Blackett katika ziara za maandalizi ya timu hiyo. Lakini suala la kuimarisha nafasi ya ulinzi limekuwa jambo muhimu kwa United baada ya kuondoka kwa mabeki wake wazoefu kama Nemanja Vidic, Rio Ferdinand na Patrice Evra katika kipindi hiki cha kiangazi. United wana uhakika wa kukamilisha usajili wa nahodha wa Arsenal Thomas Vermaelen lakini dili hilo limesimama kutokana na nia ya kocha Arsene Wenger kutaka kusajili mbadala wake kabla ya kuamua kumuuza. Akihojiwa Van Gaal amesema pamoja na kwamba mabeki alionao wameonyesha kucheza vyema lakini ni muhimu kuimarisha eneo hilo kwasababu ligi ni ndefu na kuna wakati wachezaji wanaweza kucheza chini ya kiwango kutokana na uchovu au majeruhi hivyo ni lazima kuwe na mbadala.
No comments:
Post a Comment