KIUNGO mahiri wa kimataifa wa zamani wa Brazil, Kaka amesisitiza kuwa hajutii uamuzi wake wa kujiunga na Real Madrid katika kipindi cha usajili wa kiangazi mwaka 2009 na anafikiri hakushindwa katika kipindi chote alichokuwepo Santiago Bernabeu. Nyota huyo alijiunga na Madrid akitokea AC Milan kwa ada ya paundi milioni 65 lakini hakuwahi kung’ara kama alivyotegemewa katika timu hiyo kongwe La Liga. Muda mrefu Kaka alikuwa akikaa benchi kama mchezaji wa akiba lakini bado anadai aliridhika katika muda aliokuwepo Madrid huku akiitetea rekodi yake. Kaka amesema hakushindwa wakati alipokuwa Madrid na kufafanua kuwa alicheza mechi 120 na kufunga mabao 28, hivyo kumfanya kucheza kucheza kwa wastani wa mechi 30 katika kila msimu. Nyota huyo ambaye kwasasa anacheza kwa mkopo katika timu ya Sao Paulo aliendelea kudai kuwa Jose Mourinho alimsaidia kwa kiasi kikubwa kuinua kiwango chake na kumfanya kuwa na subira. Kaka aliondoka Milan katika kipindi hiki cha kiangazi baada ya kumaliza msimu mmoja toka arejee San Siro akitokea Madrid na sasa amesaini mkataba wa mwaka mmoja na timu ya Orlando City ya Marekani ambayo nayo imempeleka kwa mkopo Sao Paulo mpaka mwakani.
No comments:
Post a Comment