Saturday, April 21, 2012

EL MAAMRY, NDOLANGA WAULA TFF.

WENYEVITI wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Said Hamad El Maamry na Muhiddin Ahmad Ndolanga wameteuliwa kuwa Marais wa heshima wa shirikisho hilo, katika Mkutano Mkuu wa TFF unaoendelea kwenye ukumbi wa NSSF Water Front, Dar es Salaam. Habari kutoka ndani ya Mkutano huo, ambao utaendelea hadi kesho, zimesema kwamba viongozi hao wa zamani nchini wamepewa heshima hiyo na Wajumbe wa Mkutano Mkuu kutokana na mchango wao katika soka ya Tanzania, enzi zao wakiwa madarakani wakati TFF ikiitwa FAT (Chama cha Soka Tanzania). Aidha, Wajumbe wa Mkutano Mkuu wameambiwa kuwa Hati ya Uwanja wa Karume haishikiliwi na benki kutokana na deni la ziara ya timu ya taifa ya Brazil Juni 2012, zaidi ya Sh. Bilioni 3, kwani deni hilo lilidhaminiwa na Serikali. Mkutano huo unatarajiwa kufungwa muda si mrefu katika siku yake ya kwanza leo, ili Wajumbe wakawahi kuangalia mechi ya timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro dhidi ya Sudan, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mkutano huo, utaendelea tena kesho katika siku ya mwisho na tarehe ya uchaguzi Mkuu, utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu, inatarajiwa kupangwa rasmi hiyo kesho.

No comments:

Post a Comment