BOSI WA RANGERS AWEKWA 'LUPANGO' MAISHA.
KLABU ya Glascow Rangers imefungiwa kusajili wachezaji kwa muda wa mwaka mmoja na mmiliki wa klabu hiyo Craig Whyte yeye amefungiwa maisha kutojishughulisha na mchezo wa soka nchini Scotland kufuatia matatizo ya kifedha yanayoikabili klabu hiyo. Rangers ambao taji la ubingwa wa Ligi Kuu nchini humo mara 54 waliingia katika mfumo wa utawala ambao ungewalinda wasifilisike Februari mwaka huu wakiwa na deni linalofikia dola milioni 14 toka Whyte alipoichukua klabu hiyo Mei mwaka jana. Mahakama ya Nidhamu ilimkuta Whyte na makosa mawili ya uvunjaji wa nidhamu kati ya Mei 6 mwaka 2011 na machi 6 2012 na kumtoza faini ya kiasi cha dola 320,000 wiki sita zilizopita ambapo Chama cha Soka cha nchi hiyo kilimuelezea kama mtu asiyefaa kujishughulisha na michezo. Kikwazo katika usajili iliyowekewa klabu hiyo kwa mwaka mmoja imekuja baada ya klabu hiyo kuvunja sheria tano za kinidhamu kwa wakati mmoja hivyo kifungo hicho kinapelekea Rangers kusajili wachezaji wa umri chini ya miaka 18 katika kipindi chote hicho cha adhabu. Rangers ambayo pia imetozwa faini ya dola 260,000 inaweza kufilisiwa kama haitapata mnunuzi mwingine ifikapo mwishoni mwa msimu huu.
No comments:
Post a Comment